Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, inatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote walioguswa na kifo cha marehemu Daudy Amosi Mwimazi, aliyepoteza maisha katika tukio lililotokea katika Kijiji cha Madibila, Kata ya Mambwekenya, Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa.
Ofisi ya Mbunge inalaani vikali kitendo cha baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, ikiwemo kuchoma gari lililokuwa limewabeba vijana waliokuwa wakifanya shughuli za kusajili laini za simu za Halotel, pamoja na kumpiga hadi kufariki dunia kijana huyo kwa tuhuma za kutoa sehemu za siri za wanaume, jambo ambalo linapaswa kuchunguzwa na kuthibitishwa na vyombo vya sheria.
Ofisi ya Mbunge inawakumbusha wananchi kuwa hakuna mtu anayepaswa kujichukulia sheria mkononi. Endapo mtu anatuhumiwa kufanya kosa, anapaswa kufikishwa katika vyombo vya sheria ili uchunguzi ufanyike na hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Wananchi wa Kalambo wanahimizwa kuendelea kudumisha misingi ya upendo, umoja, mshikamano na amani ambayo imekuwa sehemu ya utamaduni wa jamii ya Kalambo. Ni muhimu kuhakikisha kuwa vitendo vya watu wachache haviharibu taswira nzuri ya Kalambo na wananchi wake.
Aidha, Ofisi ya Mbunge inaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na wa haki ili kubaini wote waliohusika na tukio hilo na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake. Ofisi pia inawasihi wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuwabaini wahusika wote, huku wakihakikisha kuwa raia wasiohusika hawaathiriki.
Kwa kuhitimisha, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalambo inawaomba wananchi wote kuendelea kudumisha upendo, ushirikiano, mshikamano na amani, pamoja na kushirikiana kupinga vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge, Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment