Katika kutekeleza ahadi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kutoa shilingi bilioni 200 kwa vijana ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inautangazia umma kuanza kwa Awamu ya Pili ya utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana.
Malengo ya mikopo hiyo ni kuwawezesha vijana kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara ndogo, biashara za kati na kampuni changa ili kujijengea kipato katika Sekta za Mifugo na Uvuvi.
Mikopo hiyo itatolewa kwa njia ya vifaa na pembejeo za uzalishaji, ikiwemo ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa kuku (chotara, mayai na nyama), mbuzi, kondoo na nguruwe, pamoja na boti za kuhudumia vizimba, boti za uvuvi, zana za uvuvi, mifumo ya ubari (cold chain) katika mazao ya uvuvi, mifumo ya kulazisha vifaranga vya samaki, mifumo na vifaa vya uchakataji wa mazao ya uvuvi ikijumuisha makausho ya dagaa na mwani (dryers).
Vigezo na maelekezo kwa waombaji ni kama ifuatavyo:
i. Barua ya maombi na fomu ya maombi iliyojazwa;
ii. Awe na umri kati ya miaka 18 hadi 35;
iii. Awe mkazi wa eneo utakapofanyika mradi husika na awe na barua ya uthibitisho kutoka kwa Mtendaji wa Serikali za Mitaa/Vijiji
iv. Awe na uthibitisho wa kuwa raia wa Tanzania (Kitambulisho cha Taifa - NIDA, au Namba ya NIDA, kadi ya mpiga kura, leseni ya udereva, cheti cha kuzaliwa, hati ya kusafiria);
v. Mwombaji anaweza kuomba kama mtu binafsi, kampuni ya vijana, Chama cha ushirika, au kikundi kilichosajiliwa na Halmashauri husika;
vi. Awe na barua na vitambulisho (NIDA) vya wadhamini wawili (2) wanaotambulika kwenye uongozi wa Serikali ambao watawajibika kulipa deni endapo mnufaika atakiuka masharti ya mkopo huu;
vii. Awe na andiko lenye kuelezea mahitaji ya mradi kulingana na mradi uliotajwa kwenye tangazo hili;
viii. Asiwe na mikopo chechefu kutoka katika taasisi za fedha au taasisi yoyote nchini; na
ix. Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) kwa kampuni.
Inasisitizwa waombaji wawasilishe maombi yao yaliyokamilika kulingana na vigezo vilivyotolewa. Maombi yote yawasilishwe katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika kabla au ifikapo tarehe 14 Septemba, 2026. Fomu ya maombi imeambatishwa. Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia namba ya huduma kwa wateja 0737-476937.
Imetolewa na;
KATIBU MKUU
Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Mji wa Serikali Mtumba,
S. L. P. 2870,
40487 DODOMA
Barua pepe: [email protected]
KWA WANAKALAMBO:
Kwa maelekezo zaidi wasiliana na Afisa Uvuvi Wilaya kwa namba +255 767 076 267.


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment