📰 HABARI MPYA
Inapakia habari...

MIEZI 5 YA UONGOZI WA MHE. EDEFONCE JOACKIM KANONI: HATUA ZA MAENDELEO KALAMBO

MIEZI 5 YA UONGOZI WA MHE. EDEFONCE JOACKIM KANONI: HATUA ZA MAENDELEO KALAMBO

 


Ndugu wananchi wa Kalambo,

Muda wa kampeni umekwisha, sasa ni wakati wa kuungana, kushirikiana na kushikamana katika kuijenga Kalambo yetu. Maendeleo hayaletwi na mtu mmoja pekee, bali ni matokeo ya ushirikiano wa wananchi wote. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa sehemu ya safari ya maendeleo ya Wilaya ya Kalambo.

Maendeleo si jukumu la Mbunge peke yake, bali ni wajibu wa kila mwananchi. Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere:

"Kabla hujauliza Taifa lako limekufanyia nini, jiulize wewe umelifanyia nini Taifa lako."

Nasi tujiulize: Je, tumefanya nini kuijenga Kalambo yetu?

Kazi kuu za Mbunge ni kuwakilisha wananchi, kutetea maslahi yao na kutunga sheria. Katika kipindi cha miezi mitano tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonce Joackim Kanoni ameendelea kutekeleza majukumu hayo kwa bidii, uwajibikaji na uzalendo.

Mara baada ya kuchaguliwa, alifanya ziara katika kata zote 23 za Jimbo la Kalambo kwa lengo la kuwashukuru wananchi na kukusanya kero pamoja na changamoto zao ili kuziwasilisha katika mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi. Katika kipindi hicho cha miezi mitano, amechangia mara 18 Bungeni akiwasilisha hoja, kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Kalambo.

Miongoni mwa masuala aliyowasilisha Serikalini ni pamoja na umaliziaji wa magofu 143 ya vyumba vya madarasa, magofu 13 ya zahanati, umaliziaji wa vituo vya afya vinne, ukarabati wa zahanati na vituo vya afya chakavu, ujenzi wa vituo vya afya 15 katika kata ambazo hazina vituo vya afya, pamoja na ujenzi wa shule za sekondari nne katika kata ambazo bado hazina shule za sekondari.

Pia amewasilisha maombi ya kukamilisha miradi ya maji iliyokwama baada ya kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani, matengenezo ya barabara zote za Halmashauri, ujenzi wa Daraja la Mto Saise lenye urefu wa mita 80, ujenzi wa kilomita 10 za barabara za lami katika Mji wa Matai, ujenzi wa Barabara ya Mpombwe–Kipwa, upatikanaji wa fedha za kukamilisha Barabara ya Matai–Kasesya, ujenzi wa Stendi Mpya ya Matai Ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kalambo pamoja na ukarabati wa Bandari ya Kasanga.

Kutokana na jitihada hizo, Serikali imefanikiwa kutenga shilingi milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ulumi, zimeingia shilingi milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kanyezi,  Zimepangwa Fedha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kumalizia Kituo cha Afya Mwazye, Kituo cha afya Legezamwendo, Imetengwa shilingi milioni 138 Umaliziaji wa Kituo cha afya Kanyezi na  shilingi milioni 106 kwa ajili ya Umaliziaji wa Zahanati ya Kijiji cha Tunyi. Pia Zimepangwa milioni 60 mapato ya ndani kwajili ya Umaliziaji kituo cha afya Samazi.

Vilevile, shilingi milioni 172 zimepatikana kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji katika Kata ya Mbuluma huku zikiwa zimetengwa fedha za kukamilisha mradi wa maji Legezamwendo.

Kwa upande wa miundombinu, shilingi milioni 300 zimepatikana kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa Stendi Mpya ya Matai. Aidha, shilingi bilioni 1.7 tayari zimepatikana kwa ajili ya ukarabati wa barabara mbalimbali katika Wilaya ya Kalambo na kazi zinaendelea.

Fedha za kuendeleza ujenzi wa Barabara ya Matai–Kasesya tayari zimepatikana na mkandarasi anaendelea na utekelezaji wa kazi kwa kipande cha kwanza kipande cha pili zimetengwa fedha. Kadhalika, fedha za ujenzi wa barabara ya kiwango cha Nzege kutoka Rami kuelekea Bandari ya Kasanga zilishapatikana na kazi imekamilika.

Fedha zote zilizo tengwa tunazitegemea kuingizwa baada ya kupitishwa bajeti ya 2026-2027

Kwa upande wa Bandari ya Kasanga, fedha za ujenzi wa nguzo za kingo za bandari zimesha patikana mkandarasi anatafutwa aweze kuanza kazi. Aidha, Mhe. Kanoni ameendelea kujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuhamasisha matumizi ya Bandari ya Kasanga katika usafirishaji wa mizigo na biashara za kikanda.

Mhe. Kanoni pia ameendelea kutoa msukumo mkubwa katika kukamilisha Soko la Wilaya ambalo tayari limefunguliwa na kwa sasa limekamilika kwa zaidi ya asilimia 70. Baada ya Bajeti ya Serikali Kalambo pia inatarajia kupata fedha za ujenzi wa kilomita tatu za barabara ya lami ndani ya Mji wa Matai.

Katika sekta ya usafiri wa majini, ameendelea kufuatilia kwa karibu ukamilishaji wa meli ya MV Liemba ambayo kwa sasa imefikia takribani asilimia 65 ya ukamilishaji.

Kupitia Mfuko wa Jimbo, shilingi milioni 173 zimepatikana na kutumika kununua bati na saruji kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Fedha hizo zimewezesha uezekaji wa masoko katika vijiji 12, umaliziaji wa vyumba 20 vya madarasa, umaliziaji wa ofisi moja ya kijiji, ujenzi wa kivuko, umaliziaji wa matundu saba ya vyoo pamoja na umaliziaji wa ofisi moja ya kata.

Katika upande wa utetezi wa wananchi, Mhe. Kanoni amefanikisha wakulima wa Mambwe kupata mikopo ya kilimo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3. Pia ameendelea kusaidia vijana na wanawake kupata mikopo ya fedha bajaji, pikipiki na matrekta ili kuwainua kiuchumi.

Aidha, vijana 74 wamefanikiwa kujiunga na JKT, vijana 19 wamejiunga na mafunzo ya VETA, vijana saba wamepata ajira serikalini na zaidi ya vijana 100 wamepata ajira za muda mfupi kupitia makampuni mbalimbali.

Amefanikiwa kununua blanketi 30 Shuka 30 folonya 60 vyenye thamani ya shilingi milioni 1.5 kwaajili ya Kituo Cha Afya Mwimbi. Amefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 3 kwaajili ya kusaidia Michezo na kununua vifaa vya michezo. Amefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 10 kusaidia watu wenye changamoto mbalimbali.

Mbali na hayo, amekuwa karibu na wananchi katika nyakati za shida na furaha huku akiendelea kutetea maslahi ya makundi yote ya kijamii bila ubaguzi.

Ndugu wananchi wa Kalambo, ndani ya miezi mitano tu ya uongozi wake, yapo mengi yaliyofanyika na mengi zaidi yanaendelea kufuatiliwa kwa ajili ya ustawi wa wananchi wetu. Mafanikio haya ni mwanzo wa safari ndefu ya maendeleo inayohitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu.

Mwenye macho haambiwi tazama. Yapo mengi yanayoonekana na mengine yanaendelea kufuatiliwa ili kuhakikisha Kalambo inapiga hatua kubwa zaidi za maendeleo. Tuendelee kushikamana, kumuombea afya njema Mhe. Edefonce Joackim Kanoni, kumpa ushauri wenye kujenga na kumkosoa kwa nia njema ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Kwa pamoja tunaweza kuijenga Kalambo yenye maendeleo na ustawi kwa wote.

MAENDELEO KWA VITENDO

 

Imetolewa na:

Musa Frackison Mzopola

Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kalambo

Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.

Comments

MATUKIO KWA NJIA YA PICHA

Inapakia picha...

HABARI MAARUFU

FURSA ZA MIKOPO YA VIJANA SASA HADHARANI OMBA SASA UJIKWAMUE KIUCHUMI

  Katika kutekeleza ahadi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kutoa shilingi bilioni 200 kwa vijana ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inautangazia umma kuanza kwa Awamu ya Pili ya utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana. Malengo ya mikopo hiyo ni kuwawezesha vijana kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara ndogo, biashara za kati na kampuni changa ili kujijengea kipato katika Sekta za Mifugo na Uvuvi. Mikopo hiyo itatolewa kwa njia ya vifaa na pembejeo za uzalishaji, ikiwemo ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa kuku (chotara, mayai na nyama), mbuzi, kondoo na nguruwe, pamoja na boti za kuhudumia vizimba, boti za uvuvi, zana za uvuvi, mifumo ya ubari (cold chain) katika mazao ya uvuvi, mifumo ya kulazisha vifaranga vya samaki, mifumo na vifaa vya uchakataji wa mazao ya uvuvi ikijumuisha makausho ya dagaa na mwani (dryers). Vigezo na maelekezo kwa waombaji ni kama ifuatavyo: i. Baru...

NAFASI 200 ZA AJIRA ZA MAFUNDI ZATANGAZWA KWA KAZI NCHINI SAUDI ARABIA

  Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, kwa kushirikiana na Atilis Investment Limited , inawataarifu Watanzania wenye sifa stahiki kuhusu nafasi 200 za ajira za mafundi katika sekta ya ujenzi , zilizotolewa na kampuni ya Shade Corporation Limited ya nchini Saudi Arabia. KADA ZINAZOHITAJIKA Nafasi hizo zinahusisha mafundi wa kada mbalimbali, wakiwemo: Mafundi Uashi Mafundi Useremala Wasuka Nondo SIFA ZA MWOMBAJI Mwombaji anatakiwa kuwa na: Elimu ya astashahada kutoka chuo cha ufundi kinachotambuliwa na Serikali; Uzoefu wa kazi wa miaka miwili (2) au zaidi katika sekta ya ufundi; Uwezo na uzoefu katika kada husika, ikiwemo Uashi, Useremala au Usuka Nondo; Umri kati ya miaka 21 hadi 40 ; Waombaji wa nafasi hizi wanatakiwa kuwa wanaume . MASHARTI NA MAFANO YA AJIRA Waombaji watakaofaulu mchakato wa ajira watapata fursa ya kufanya kazi nchini Saudi Arabia kwa masharti yaliyowekwa na mwajiri. Miongoni mwa mafao na masharti ya ajira ni: Mshahara wa Riyal 1...

MHE. MBUNGE KANONI ASHIRIKI MAZISHI YA WAATHIRIKA WA AJALI KAZILA, ATOA WITO WA UPENDO, UMOJA NA MSHIKAMANO

  KALAMBO: Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni , ameshiriki mazishi ya wananchi wawili waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Kazila, Kata ya Mwazye, Wilaya ya Kalambo, huku akitoa pole na faraja kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wananchi wote walioguswa na msiba huo. Ajali hiyo ilitokea tarehe 05 Agosti 2026 , wakati gari aina ya Fuso lililokuwa limebeba watu waliokuwa wakielekea kwenye shughuli ya harusi kutoka Kijiji cha Msoma, Kata ya Mwazye, Wilaya ya Kalambo , lilipofika katika Kijiji cha Kazila kwa ajili ya shughuli ya kufunga ndoa. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, gari hilo lilikuwa limembeba bwana harusi, Hosea Gilbert Watua , pamoja na watu wengine waliokuwa wakisafiri naye kutoka Kijiji cha Msoma kuelekea Kijiji cha Kazila, ambako alikuwa akienda kufunga ndoa na bibi harusi, Mehili Sauli Visent , mkazi wa Kijiji cha Kazila, Kata ya Mwazye. AJALI YATOKEA KABLA YA KUFIKA KWENYE DARAJA Taarifa zinaeleza ...