📰 HABARI MPYA
Inapakia habari...

MIKOPO YA HALMASHAURI SIYO BAHATI – NI FURSA INAYOHITAJI MAANDALIZI: ELEWA KWANZA, KISHA FANIKIWA

MIKOPO YA HALMASHAURI SIYO BAHATI – NI FURSA INAYOHITAJI MAANDALIZI: ELEWA KWANZA, KISHA FANIKIWA

 

Wananchi wenzangu wa Jimbo la Kalambo,

Kumekuwa na maswali mengi kuhusu mikopo inayotolewa na Serikali na Halmashauri. Wapo wanaoamini kuwa mikopo haitoki, wengine hudhani masharti ni magumu, na wengine huanzisha vikundi kwa lengo la kusubiri fedha za mkopo pekee. Ukweli ni kwamba, mafanikio ya kupata mkopo huanza na kuwa na uelewa sahihi wa mfumo wa utoaji wake.

Aina za mikopo inayotolewa na Serikali

Kwa ujumla, kuna aina kuu tatu za mikopo inayowezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

1. Mikopo ya Wizara

Hii imegawanyika katika makundi mawili:

  • Mikopo isiyo na riba inayotolewa kupitia Wizara inayosimamia maendeleo ya jamii.
  • Mikopo yenye riba ya asilimia 5 inayotolewa kupitia wizara mbalimbali za kisekta kwa ajili ya shughuli maalumu za kiuchumi.

2. Mikopo ya Wajasiriamali Wadogo

Hii hutolewa kupitia taasisi za benki kwa wajasiriamali wadogo na kwa kawaida huwa na riba ya takribani asilimia 7 kulingana na utaratibu wa mpango husika.

3. Mikopo ya Halmashauri (Asilimia 10)

Hii ni mikopo isiyo na riba, na ndiyo ambayo wananchi wengi huizungumza. Hata hivyo, ipo haja ya kuifahamu kwa undani ili kuondoa dhana potofu zilizojengeka.

Ukweli kuhusu Mikopo ya Halmashauri

Jambo la kwanza ambalo kila mwananchi anatakiwa kulielewa ni kwamba, hakuna fedha zinazokuwa zimekaa pembeni zikisubiri wakopaji.

Fedha za mikopo ya Halmashauri hutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri. Kadiri mapato yanavyoongezeka, ndivyo kiwango cha fedha za mikopo kinavyoongezeka pia.

Hivyo, kiasi cha fedha kinachotolewa hutegemea mapato halisi yaliyopatikana katika kipindi husika.

Utaratibu wa utoaji wa mikopo

Kwa kawaida, kila baada ya miezi mitatu Halmashauri hufungua dirisha la maombi ya mikopo.

Utaratibu huwa kama ifuatavyo:

  • Halmashauri hutoa tangazo rasmi la mikopo na kutangaza kiasi cha fedha kilichopo kwa ajili ya kukopesha.
  • Wananchi hupewa takribani mwezi mmoja kuwasilisha maombi.
  • Baada ya muda wa maombi kuisha, Halmashauri hutumia mwezi mmoja kukagua vikundi na miradi yao.
  • Siku 15 hutumika kutembelea na kuhakiki miradi.
  • Siku 15 zinazofuata hutumika kuidhinisha na kutoa mikopo kwa vikundi vilivyokidhi vigezo.

Nani anastahili kuomba?

Mikopo hii hutolewa kwa:

  • Vikundi vya Vijana.
  • Vikundi vya Wanawake.
  • Vikundi vya Watu wenye Ulemavu.

Ili kikundi kipate mkopo lazima:

  • Kiwe kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.
  • Kiwe na mradi unaoendelea na unaoonekana kufanya kazi.
  • Kiwasilishe barua ya maombi.
  • Kiambatishe mpango wa matumizi ya fedha na namna zitakavyokuza mradi.
  • Kiambatishe muhtasari wa kikao unaoonyesha wanakikundi wamekubaliana kuomba mkopo.

Kwa nini baadhi ya vikundi havipati mkopo?

Zipo sababu kuu mbili:

Kwanza, kikundi kutokukidhi vigezo vilivyowekwa.

Pili, fedha zilizopo zinaweza kuwa ndogo kuliko mahitaji ya waombaji.

Kwa mfano, kama Halmashauri ina shilingi milioni 100 za kukopesha lakini maombi yote yanafikia milioni 300, ni wazi kuwa si kila kikundi kitapata mkopo katika awamu hiyo. Vikundi vitakavyokosa si kwamba havistahili, bali vitasubiri dirisha litakalofuata kulingana na fedha zitakazopatikana.

Changamoto kubwa iliyopo

Wananchi wengi bado hawajapata elimu ya kutosha kuhusu mfumo huu wa mikopo.

Wengi huanzisha vikundi kwa lengo la kupata mkopo pekee, badala ya kuanza kujenga shughuli za kiuchumi kwa nguvu zao. Wanapofika hatua ya ukaguzi hukosa sifa kwa sababu hawana mradi unaoendelea. Baada ya kukosa mkopo, vikundi huvunjika na kuanza kusema kuwa masharti ni magumu au fedha hazitoki.

Huo si ukweli.

Mkopo unalenga kuimarisha biashara au mradi uliopo, si kuanzisha ndoto ambayo bado haijaanza kutekelezwa.

Wito kwa Wanakalambo

Ndugu zangu Wanakalambo, ni wakati wa kubadili mtazamo.

Tusiunde vikundi kwa ajili ya kusubiri mkopo pekee. Tuanzishe miradi, tushirikiane, tutoe mchango wetu na tujenge msingi imara wa kujitegemea. Kikundi kinachoonyesha uwezo wa kufanya kazi kina nafasi kubwa zaidi ya kupata mkopo na hata kuurejesha kwa mafanikio.

Tusisubiri fedha zitubadilishe maisha; tuanze sisi kubadili maisha yetu, kisha fedha zitakuwa nyenzo ya kutuongezea nguvu.

Kumbukeni, hakuna mafanikio bila juhudi.

Anza leo. Amini unaweza. Ondoa fikra za kusema "siwezi" na ujenge imani ya kusema "naweza." Mtazamo huo ndiyo hatua ya kwanza kuelekea mafanikio ya kiuchumi kwa mtu binafsi, kikundi na jamii kwa ujumla.

Imetolewa na:

Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge, Jimbo la Kalambo


Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.

Comments

MATUKIO KWA NJIA YA PICHA

Inapakia picha...

HABARI MAARUFU

FURSA ZA MIKOPO YA VIJANA SASA HADHARANI OMBA SASA UJIKWAMUE KIUCHUMI

  Katika kutekeleza ahadi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kutoa shilingi bilioni 200 kwa vijana ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inautangazia umma kuanza kwa Awamu ya Pili ya utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana. Malengo ya mikopo hiyo ni kuwawezesha vijana kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara ndogo, biashara za kati na kampuni changa ili kujijengea kipato katika Sekta za Mifugo na Uvuvi. Mikopo hiyo itatolewa kwa njia ya vifaa na pembejeo za uzalishaji, ikiwemo ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa kuku (chotara, mayai na nyama), mbuzi, kondoo na nguruwe, pamoja na boti za kuhudumia vizimba, boti za uvuvi, zana za uvuvi, mifumo ya ubari (cold chain) katika mazao ya uvuvi, mifumo ya kulazisha vifaranga vya samaki, mifumo na vifaa vya uchakataji wa mazao ya uvuvi ikijumuisha makausho ya dagaa na mwani (dryers). Vigezo na maelekezo kwa waombaji ni kama ifuatavyo: i. Baru...

NAFASI 200 ZA AJIRA ZA MAFUNDI ZATANGAZWA KWA KAZI NCHINI SAUDI ARABIA

  Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, kwa kushirikiana na Atilis Investment Limited , inawataarifu Watanzania wenye sifa stahiki kuhusu nafasi 200 za ajira za mafundi katika sekta ya ujenzi , zilizotolewa na kampuni ya Shade Corporation Limited ya nchini Saudi Arabia. KADA ZINAZOHITAJIKA Nafasi hizo zinahusisha mafundi wa kada mbalimbali, wakiwemo: Mafundi Uashi Mafundi Useremala Wasuka Nondo SIFA ZA MWOMBAJI Mwombaji anatakiwa kuwa na: Elimu ya astashahada kutoka chuo cha ufundi kinachotambuliwa na Serikali; Uzoefu wa kazi wa miaka miwili (2) au zaidi katika sekta ya ufundi; Uwezo na uzoefu katika kada husika, ikiwemo Uashi, Useremala au Usuka Nondo; Umri kati ya miaka 21 hadi 40 ; Waombaji wa nafasi hizi wanatakiwa kuwa wanaume . MASHARTI NA MAFANO YA AJIRA Waombaji watakaofaulu mchakato wa ajira watapata fursa ya kufanya kazi nchini Saudi Arabia kwa masharti yaliyowekwa na mwajiri. Miongoni mwa mafao na masharti ya ajira ni: Mshahara wa Riyal 1...

MHE. MBUNGE KANONI ASHIRIKI MAZISHI YA WAATHIRIKA WA AJALI KAZILA, ATOA WITO WA UPENDO, UMOJA NA MSHIKAMANO

  KALAMBO: Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni , ameshiriki mazishi ya wananchi wawili waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Kazila, Kata ya Mwazye, Wilaya ya Kalambo, huku akitoa pole na faraja kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wananchi wote walioguswa na msiba huo. Ajali hiyo ilitokea tarehe 05 Agosti 2026 , wakati gari aina ya Fuso lililokuwa limebeba watu waliokuwa wakielekea kwenye shughuli ya harusi kutoka Kijiji cha Msoma, Kata ya Mwazye, Wilaya ya Kalambo , lilipofika katika Kijiji cha Kazila kwa ajili ya shughuli ya kufunga ndoa. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, gari hilo lilikuwa limembeba bwana harusi, Hosea Gilbert Watua , pamoja na watu wengine waliokuwa wakisafiri naye kutoka Kijiji cha Msoma kuelekea Kijiji cha Kazila, ambako alikuwa akienda kufunga ndoa na bibi harusi, Mehili Sauli Visent , mkazi wa Kijiji cha Kazila, Kata ya Mwazye. AJALI YATOKEA KABLA YA KUFIKA KWENYE DARAJA Taarifa zinaeleza ...