MTULA, KATA YA MNAMBA, KALAMBO — 08 AGOSTI 2026
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Musa Frackison Mzopola, amemwakilisha Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, katika hafla ya kuhitimisha mashindano ya mpira wa miguu ya Malingumu Cup, yaliyofanyika katika Kijiji cha Mtula, Kata ya Mnamba, Wilaya ya Kalambo.
Musa alishiriki katika hafla hiyo kama Mgeni Rasmi, ambapo alikabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo yaliyokuwa yamezinduliwa na Mhe. Mbunge Kanoni tarehe 02 Juni 2026 katika Kijiji cha Luse, na kuhitimishwa tarehe 08 Agosti 2026 katika Kijiji cha Mtula, Kata ya Mnamba.
Katika uzinduzi wa ligi hiyo, Mhe. Mbunge Kanoni aliahidi kuchangia shilingi milioni moja, kuongeza kwenye kiasi cha shilingi milioni moja kilichoandaliwa na Mhe. Kassim Lupia Simchimba, Diwani wa Kata ya Mnamba na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kalambo, kwa ajili ya zawadi kwa washindi.
Kwa mujibu wa mpangilio wa zawadi, mshindi wa kwanza alipokea shilingi milioni moja, mshindi wa pili shilingi laki tano, huku mshindi wa tatu akipokea shilingi laki mbili na nusu.
Fedha nyingine zilitolewa kwa washiriki waliotambuliwa katika vipengele mbalimbali vya mashindano hayo, ikiwemo mchezaji bora, mchezaji mwenye nidhamu, mfungaji bora na kipa bora.
MUSA: “MBUNGE KANONI NI MBUNGE WA VITENDO, SIO MANENO”
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mashindano hayo, Katibu wa Mbunge, Musa Frackison Mzopola, aliwasilisha salamu za Mhe. Kanoni kwa wananchi wa Mnamba na Kalambo kwa ujumla, akisisitiza kuwa Mbunge huyo ni kiongozi anayetekeleza yale anayoyaahidi.
Musa alisema:
“Mhe. Mbunge ni Mbunge wa vitendo, sio maneno. Anachoongea anatenda, sio mbabaishaji.”
Alisema Mhe. Kanoni amekuwa akionesha kwa vitendo dhamira yake ya kushirikiana na wananchi na kuunga mkono shughuli mbalimbali zinazolenga kuleta maendeleo, kuimarisha umoja na kukuza vipaji vya vijana.
Musa aliwakumbusha wananchi kuwa wakati wa uzinduzi wa Malingumu Cup, Mhe. Kanoni aliahidi kuchangia shilingi milioni moja, ahadi ambayo imetekelezwa na fedha hizo kufikishwa kwa ajili ya kugawanywa kwa washindi kwa mujibu wa mpangilio uliowekwa.
Kuhusu ahadi ya jezi kwa washindi, Musa alisema Mhe. Kanoni tayari aliagiza jezi hizo kutoka China, lakini hadi wakati wa kuhitimisha ligi zilikuwa bado hazijawasili. Hivyo, aliwaomba wananchi na washiriki kuwa na subira hadi zitakapofika.
MUSA AWAPONGEZA WANANCHI NA WAANDAAJI WA LIGI
Katibu wa Mbunge aliwapongeza wananchi wa Mnamba kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia hitimisho la ligi hiyo, akisema mwitikio wao umeonesha upendo na nia ya dhati ya wananchi katika kuendeleza michezo.
Pia aliwapongeza wachezaji kwa kujituma, kucheza vizuri, kuonyesha nidhamu na kuvumilia changamoto tangu mwanzo wa ligi hadi hatua ya mwisho.
Aidha, Musa aliwashukuru kwa dhati watu wote walioshiriki katika kuandaa, kuratibu na kufanikisha Malingumu Cup, akisema mafanikio ya ligi hiyo yametokana na ushirikiano wa wananchi, viongozi, waandaaji, wachezaji na wadau mbalimbali.
Aliwasihi wachezaji na vijana kwa ujumla kutokata tamaa katika safari ya mafanikio, akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji juhudi, uvumilivu, nia na malengo.
“Msivunjike moyo. Mafanikio huja kwa kupambana. Ukiwa na nia na malengo, itakusaidia kutimiza ndoto zako.”
MUSA AWAPONGEZA WANANCHI KWA KUMCHAGUA DIWANI KASSIM
Musa aliwapongeza wananchi wa Kata ya Mnamba kwa kumchagua Mhe. Kassim Lupia Simchimba kuwa Diwani, akimtaja kuwa ni kiongozi mchapakazi, mzalendo, mwajibikaji na mwenye hofu ya Mungu, ambaye amekuwa mfano wa kuigwa ndani ya Wilaya ya Kalambo.
Alisema sifa hizo ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Mhe. Kassim, mara baada ya kuchaguliwa kuwa Diwani kwa awamu yake ya kwanza, kuaminiwa na kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kalambo.
Musa pia alimpongeza Mhe. Kassim kwa namna anavyowapenda na kuwathamini wananchi wa Mnamba na Kalambo kwa ujumla, akisema kuwa maandalizi na udhamini wa Malingumu Cup ni mfano wa namna viongozi wanavyoweza kutumia nafasi zao kuunga mkono vipaji vya vijana na kuimarisha umoja katika jamii.
DAUDI SENGO AELEZA UPENDO WA DIWANI KWA WANANCHI WA MNAMBA
Kwa upande wake, Ndugu Daudi Sengo, Mratibu wa Elimu Kata ya Mnamba, alieleza namna Diwani wa Kata ya Mnamba, Mhe. Kassim Lupia Simchimba, anavyowapenda na kuwathamini wananchi wa Mnamba.
Daudi alisema Mhe. Kassim amekuwa akionesha kwa vitendo dhamira yake ya kuunga mkono shughuli za wananchi, ikiwemo kuendesha mashindano hayo ambayo yalihitaji gharama kubwa.
Alieleza kuwa Mhe. Diwani ameingia katika gharama kubwa kuhakikisha ligi hiyo inafanyika na kufikia tamati kwa mafanikio, jambo alilolieleza kuwa ni ishara ya upendo na kuthamini wananchi pamoja na vijana wanaopenda michezo.
Kwa niaba ya Mhe. Kassim Lupia Simchimba, Daudi alitoa shukrani za dhati kwa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalambo kwa kushiriki katika hafla hiyo na kuwaunga mkono wananchi wa Mnamba.
Alisema ushiriki wa Ofisi ya Mbunge katika ligi hiyo umeonesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi na wananchi katika kuendeleza shughuli za kijamii na michezo.
MHE. REHEMA AWAPONGEZA WANANCHI NA DIWANI KASSIM
Katika ziara hiyo, Katibu wa Mbunge aliambatana na Mhe. Rehema Gospel Limba, Diwani Viti Maalum Tarafa ya Mwimbi, ambaye pia aliwapongeza wananchi kwa kuandaa na kufanikisha mashindano hayo.
Mhe. Rehema aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na pia kwa kumchagua Mhe. Kassim Lupia Simchimba kuwa Diwani wa Kata ya Mnamba, akimtaja kuwa kiongozi anayejituma katika kuwahudumia wananchi.
MHE. KANONI AWASALIMIA WANANCHI WA MNAMBA
Musa aliwaeleza wananchi kuwa Mhe. Kanoni alikusudia kufika mwenyewe katika hafla ya kuhitimisha Malingumu Cup, lakini kutokana na majukumu ya Serikali yaliyomlazimu kuwa nje ya eneo hilo, alimtuma Katibu wake kwenda kumwakilisha.
Aliwasilisha salamu za Mhe. Kanoni kwa wananchi wa Mnamba na kusema kuwa Mbunge huyo anawapenda, anawathamini na anaendelea kuwa pamoja nao katika shughuli za maendeleo.
Musa alisema Mhe. Kanoni aliwashukuru wananchi kwa heshima kubwa waliyompatia kwa kumualika kushiriki katika uzinduzi wa ligi hiyo, pamoja na kumchagua kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalambo na kuamua kushirikiana naye katika kuleta maendeleo.
Alisisitiza kuwa Mhe. Kanoni alitamani sana kufika na kushiriki pamoja na wananchi katika hitimisho la ligi hiyo, lakini majukumu ya Serikali yalimlazimu kutokuwepo.
Baada ya hotuba hizo, Katibu wa Mbunge, Musa Frackison Mzopola, alikabidhi zawadi kwa washindi na washiriki waliotambuliwa katika vipengele mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kufunga rasmi mashindano ya Malingumu Cup 2026.
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge, Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment