Dodoma: Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, ameibana Serikali kuhusu uboreshaji wa huduma za afya katika Jimbo la Kalambo, akitaka hatua zichukuliwe kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Mhe. Kanoni ametoa kauli hiyo wakati akiuliza swali la nyongeza Bungeni, ambapo aliishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ulumi, hatua ambayo itasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Hata hivyo, Mhe. Kanoni alitaka Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasanga, ambayo iliwahi kutolewa na Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge Kanoni aliuliza ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasanga, ili wananchi wa Kata ya Kasanga waweze kupata huduma za afya kwa urahisi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Akijibu swali hilo, Prof. Liziki Shemdoe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, alimpongeza Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni kwa jitihada zake za kuendelea kuwapambania wananchi wa Kalambo pamoja na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Prof. Shemdoe alisema Serikali inaendelea kuandaa na kutenga fedha hatua kwa hatua, na kwamba fedha zitakapopatikana kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasanga, ujenzi utaanza ili kutekeleza na kukamilisha ahadi hiyo.
Kauli hiyo ya Serikali imeendelea kutoa matumaini kwa wananchi wa Kata ya Kasanga, ambao wamekuwa wakihitaji huduma ya afya inayopatikana karibu na maeneo yao.
Mhe. Kanoni ameendelea kusisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya na kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Jimbo la Kalambo.
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment