Katibu wa Mbunge Jimbo la Kalambo, Ndugu Musa Frackison Mzopola, ametembelea Kijiji cha Ulumi katika utekelezaji wa mpango wa Ofisi ya Mbunge wa kutembelea vijiji na vitongoji vya Jimbo la Kalambo, kutembea mtaa kwa mtaa, kusikiliza kero na changamoto za wananchi na kushirikiana na viongozi kuzitafutia ufumbuzi.
Akiwa Ulumi, Musa alizunguka katika mitaa mbalimbali na kuzungumza na wananchi, kuwasikiliza na kuwaalika kuendelea kutumia Ofisi ya Mbunge kama sehemu ya kuwasilisha kero, changamoto na maoni yao kuhusu maendeleo ya maeneo yao.
Musa pia aliwaeleza wananchi kuhusu mpango wa Ofisi ya Mbunge wa kuanzisha Dawati la Maoni, litakalotoa nafasi kwa mwananchi kuwasilisha kero au changamoto yake akiwa katika eneo lolote alipo.
Katika kurahisisha utoaji wa kero hizo, Ofisi ya Mbunge imeandaa mfumo wa uwasilishaji wa kero kupitia tovuti yake. Wananchi wenye simu janja wanaweza kutumia mfumo huo kuwasilisha changamoto zao, huku wale ambao hawana simu janja wakiweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa kutumia simu za kawaida.
Musa alisema mpango huo unalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya kufikisha kero zao Ofisini kwa Mbunge bila kujali mahali wanapoishi, huku Ofisi ikiendelea na mpango wa kutembelea vijiji na vitongoji vyote vya Jimbo la Kalambo.
WANANCHI WAWASILISHA KERO NA CHANGAMOTO
Katika ziara hiyo, wananchi waliwasilisha changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa madawati shuleni, wafugaji wanaoingia katika maeneo ya wakulima bila kufuata taratibu, ukosefu wa stendi ya magari, changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na baadhi ya watendaji kutowajibika ipasavyo na kutokuwa na mahusiano mazuri na wananchi.
Wananchi pia waliwasilisha changamoto ya mfereji wa kuzuia maji kuelekea katika soko la kijiji, pamoja na changamoto ya bei ya mahindi na vipimo vinavyotumika katika ununuzi wa mazao.
OFISI YA MBUNGE YAANZA KUFANYIA KAZI SUALA LA MFEREJI
Akijibu changamoto zilizolenga Ofisi ya Mbunge, hususan suala la mfereji wa kuzuia maji kuelekea katika soko la kijiji, Musa aliwaomba wananchi kuwa na subira na kuwahakikishia kuwa suala hilo tayari linafanyiwa kazi.
Alieleza kuwa Ofisi ya Mbunge tayari iliwasiliana na viongozi wa kijiji na kuwaomba kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa mfereji huo.
Tathmini hiyo tayari imefanyika na kuwasilishwa Ofisini kwa Mbunge, na kwa sasa inaandaliwa bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi huo.
Musa aliwahakikishia wananchi kuwa Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni yupo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, akisisitiza kuwa wananchi ndio waliompa dhamana ya kuwawakilisha.
Aidha, aliwaeleza kuwa Mhe. Mbunge ameahidi kuhakikisha suala la mfereji huo linapatiwa ufumbuzi kabla ya msimu wa mvua kuanza.
MIKOPO: MUSA AWATAKA WANANCHI KUTUMIA FURSA ZA BENKI
Kuhusu changamoto ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, Musa alieleza kuwa mikopo inayotolewa na Halmashauri inategemea makusanyo ya Halmashauri, ambapo asilimia 10 ya makusanyo hutengwa kwa ajili ya mikopo hiyo.
Alisema Halmashauri ya Kalambo ina vyanzo vichache vya mapato, hivyo kiasi kinachokusanywa wakati mwingine hakitoshelezi mahitaji ya vikundi vyote vinavyoomba mikopo.
Kutokana na hali hiyo, aliwashauri wananchi na vikundi kutanua wigo wa kutafuta mitaji na kutumia fursa zinazotolewa na taasisi za fedha badala ya kutegemea mikopo ya Halmashauri pekee.
Musa alitoa mfano wa mkopo wa wajasiriamali wadogo unaotolewa na CRDB Bank, akieleza masharti aliyowasilisha kwa wananchi kuwa mwombaji anatakiwa kuwa katika kikundi kilichosajiliwa, kila mwanakikundi kuwa na akaunti yake pamoja na akaunti ya kikundi.
Alieleza kuwa kila mwanakikundi anatakiwa kuweka katika akaunti ya kikundi asilimia 10 ya kiasi cha mkopo anachohitaji, huku katika akaunti yake binafsi akiwa na kiasi kisichopungua Shilingi 150,000.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, mkopo huo hauna riba wala dhamana, na mwanakikundi mmoja anaweza kukopeshwa hadi Shilingi milioni 5 kwa muda wa mwaka mmoja.
Musa alifafanua pia kuwa baada ya mkopo kumalizika na marejesho kukamilika, fedha ya asilimia 10 iliyowekwa katika akaunti ya kikundi hubaki kuwa fedha ya mwanakikundi.
AFISA KILIMO WA KATA YA ULUMI ATOA UFAFANUZI KUHUSU BEI NA VIPIMO VYA MAHINDI
Katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kilimo, Musa alizungumza na Afisa Kilimo wa Kata ya Ulumi, Ndugu Hussen, ambaye alikiri kuwepo kwa changamoto ya bei ndogo ya mahindi.
Afisa huyo alisema kwa wakati huo mahindi yalikuwa yakinunuliwa kwa bei ya takribani Shilingi 40,000, huku Serikali ikitarajiwa kutangaza bei na kuanza ununuzi ndani ya mwezi Agosti.
Aliwaomba wananchi kuwa na subira huku wakisubiri hatua za Serikali kuhusu bei ya zao hilo.
Kuhusu changamoto ya vipimo, Afisa Kilimo wa Kata ya Ulumi, Ndugu Hussen, alikiri kuwa baadhi ya wanunuzi wamekuwa wakinunua gunia lenye kilo 115 badala ya kilo 100, jambo ambalo linawaumiza wakulima.
Alisema tayari wameanza kuchukua hatua kwa kufanya vikao na madalali wa mahindi, kuwapatia maelekezo na kuwashauri kujirasimisha ili iwe rahisi kuwafuatilia na kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia taratibu.
Madalali hao tayari wameunda kikundi na wameanza kufanya mikutano ya kusikiliza kero na changamoto zao pamoja na kujadiliana namna ya kuzitatua.
Afisa Kilimo wa Kata ya Ulumi alieleza pia kuwa walifanya jitihada za kuitisha kikao na wanunuzi wa mahindi ili kujadili changamoto hizo, lakini wanunuzi hawakuweza kufika kwenye kikao hicho. Hata hivyo, alisema bado wanaendelea kutumia njia nyingine za kuwafikia ili kupata suluhisho.
DIWANI WA ULUMI ATOA UFAFANUZI KUHUSU WAFUGAJI
Musa pia alizungumza na Mhe. Inyasi Palakata, Diwani wa Kata ya Ulumi, kuhusu changamoto ya wafugaji wanaoingia katika maeneo ya wakulima bila kufuata taratibu.
Diwani huyo alikiri kuwepo kwa wafugaji walioingia katika maeneo hayo bila kufuata taratibu na sheria, na kueleza kuwa tayari wameanza kuchukua hatua.
Alisema wamefanya vikao na wafugaji katika vijiji mbalimbali vya Kata ya Ulumi na hadi sasa wamebaini wafugaji watano walioingia baada ya kukaribishwa na baadhi ya wananchi, huku wengine wakidaiwa kukaribishwa na baadhi ya viongozi wa vijiji bila kufuata taratibu zinazotakiwa.
Mhe. Diwani alisema bado wanaendelea na zoezi la kubaini wafugaji walioingia kinyume cha utaratibu, huku maelekezo yakitolewa kwa wale walioingia bila kufuata sheria na taratibu kurejea walikotoka.
Aidha, alisema wale walioingia kwa mujibu wa sheria na taratibu wanaruhusiwa kuendelea na shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
UPUNGUFU WA MADAWATI
Kuhusu upungufu wa madawati, Mhe. Inyasi Palakata alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo katika shule za Kata ya Ulumi.
Alisema tayari wamefanya vikao na kuweka mikakati ya kutengeneza madawati kwa kushirikiana na wananchi ili kupunguza na hatimaye kuondoa tatizo hilo.
MPANGO WA KUJENGA STENDI YA MAGARI
Kuhusu changamoto ya msongamano wa magari, Mhe. Diwani alisema tayari wameanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kutafuta eneo litakalotumika kujenga stendi ya magari.
Alieleza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kupata eneo lililotolewa na mwananchi, ambalo lipo katika eneo la Barabara ya kuelekea Kata ya Mnamba.
Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari na kuhakikisha shughuli za usafirishaji zinafanyika katika eneo rasmi na salama.
DIWANI ATOA AHADI YA KUFANYIA KAZI MALALAMIKO YA WATENDAJI
Kuhusu malalamiko ya baadhi ya watendaji kutokuwa na mahusiano mazuri na wananchi na kutowajibika ipasavyo, Mhe. Diwani alisema amelipokea suala hilo na atalifanyia kazi.
Alisema atakutana na wahusika ili kujadili changamoto hiyo na kutafuta namna ya kuboresha mahusiano kati ya watendaji na wananchi pamoja na kuhakikisha kila mmoja anawajibika kwa mujibu wa majukumu yake.
OFISI YA MBUNGE YAOMBA WANANCHI KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO
Ofisi ya Mbunge Jimbo la Kalambo imewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, katika juhudi za kuleta maendeleo endelevu katika jimbo hilo.
Wananchi wameaswa kudumisha upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano, pamoja na kuendelea kuwasilisha kero, changamoto na mapendekezo yao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Ofisi ya Mbunge imesisitiza kuwa ziara za kutembelea vijiji na vitongoji zitaendelea, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuhakikisha sauti zao zinasikika na changamoto zao zinafanyiwa kazi.
TUMA MAONI YAKO OFISI YA MBUNGE
Simu: 0625850656
Barua pepe: [email protected]
Tovuti: www.mbungekalambo.com
KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment