Tunatoa shukrani za dhati kwa wananchi wote wanaoendelea kutoa maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kuhusu namna Ofisi ya Mbunge inavyowasiliana na kuwafikishia taarifa wananchi.
Tunathamini kila maoni yanayotolewa, kwa sababu maoni ya wananchi ni sehemu muhimu ya kujenga mawasiliano bora, uwazi na ushirikiano kati ya Ofisi ya Mbunge na wananchi.
Kuhusu matumizi ya vyanzo vya habari, si kwamba Ofisi ya Mbunge inapuuza njia nyingine za mawasiliano au maoni yanayotolewa. Kila njia ina umuhimu wake. Hata hivyo, tunapokuwa na taarifa zinazotolewa na Ofisi, tunapenda ziwe na sehemu ya kuanzia ambayo mwananchi anaweza kuirejea na kupata taarifa nzima kama ilivyotolewa.
Ndiyo maana tunaendelea kutumia vyanzo rasmi vya Ofisi pamoja na kushirikisha taarifa hizo kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp na mitandao mingine. Lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo wale ambao bado hawajafahamu vyanzo vya taarifa vya Ofisi.
UMUHIMU WA KUJUA CHANZO CHA TAARIFA
Katika kipindi hiki ambacho taarifa husambaa kwa kasi kubwa, wakati mwingine taarifa inapokuwa inapitishwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine inaweza kukatwa sehemu, kuwekewa kichwa tofauti, kuongezewa maelezo au kutolewa nje ya muktadha wake wa awali.
Hali hiyo inaweza kumfanya msomaji kupata tafsiri tofauti na taarifa iliyokusudiwa.
Kwa kuwa taarifa zinazotolewa na Ofisi ya Mbunge ni taarifa za taasisi, ni vizuri kuwepo sehemu ambayo wananchi wanaweza kurejea na kuona taarifa kamili kama ilivyotolewa, pamoja na maelezo yake katika muktadha wake.
Hii pia husaidia kuhifadhi kumbukumbu za taarifa kwa muda mrefu, kurahisisha urejeleaji na kupunguza uwezekano wa taarifa kuchanganywa au kubadilishwa wakati wa kusambazwa.
KUHUSU WAJIBU KATIKA KUSAMBAZA TAARIFA
Tunaamini kila mmoja ana nafasi muhimu katika kujenga mazingira mazuri ya mawasiliano. Sheria na kanuni zinazohusu maudhui mtandaoni zinaweka wajibu wa kutumia mitandao kwa uangalifu na kuzingatia maudhui yanayoruhusiwa.
Kwa hiyo, tunaposhirikisha taarifa, ni vizuri pia kuangalia chanzo chake na kuhakikisha taarifa haibadilishwi au kutumiwa kwa namna ambayo inaweza kumpotosha mtu mwingine au kuleta madhara.
Hili si suala la kumzuia mtu kutoa maoni au kushirikisha taarifa, bali ni sehemu ya kujenga utamaduni wa mawasiliano yenye usahihi, uwazi, heshima na uwajibikaji.
KUHUSU MATUMIZI YA BANDO
Tunatambua pia changamoto ya gharama za intaneti na matumizi ya bando. Kwa hiyo, tunaomba radhi kwa usumbufu wowote ambao unaweza kujitokeza wakati wa kutumia njia zetu za kidijitali.
Tovuti ya Ofisi ya Mbunge imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji mbalimbali, wakiwemo wananchi wanaotumia vifurushi vidogo vya intaneti au waliopo katika maeneo yenye internet yenye kasi ndogo.
Muundo wake umezingatia matumizi bora ya data na kurahisisha upatikanaji wa taarifa. Hivyo, hata ukiwa na MB chache au ukiwa katika eneo lenye internet yenye kasi ndogo, bado unaweza kufungua na kusoma taarifa za Ofisi.
Tunataka wananchi wawe na utulivu katika kutumia tovuti hiyo. Lengo si kutumia kiasi kikubwa cha bando, bali kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi wengi zaidi.
TOVUTI YA OFISI YA MBUNGE
Kwa wananchi ambao bado hawajafahamu, tunapenda kuwajulisha kuhusu tovuti ya Ofisi ya Mbunge Jimbo la Kalambo:
🌐 www.mbungekalambo.com
Tovuti hii ni sehemu muhimu ya kupata taarifa na kumbukumbu za shughuli zinazohusiana na Ofisi ya Mbunge Jimbo la Kalambo.
Wananchi wako huru kutumia njia yoyote inayowafaa kupata taarifa. Hata hivyo, pale wanapohitaji taarifa kamili kutoka Ofisi ya Mbunge, tovuti hii inaweza kuwa sehemu nzuri ya kuanzia na kurejea taarifa hizo.
Tunawashukuru sana wananchi wote kwa maoni, ushauri, maswali na mapendekezo yenu. Tunathamini ushirikiano wenu na tutaendelea kusikiliza na kuboresha namna tunavyowafikishia taarifa.
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment