Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, amekutana na kufanya kikao na Machifu wa Wilaya ya Kalambo, ambapo pamoja na mambo mengine, amewashukuru Machifu hao kwa baraka, ushauri na ushirikiano wao, pamoja na mchango wao katika safari yake ya kuingia katika nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kalambo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kanoni amewashukuru Machifu kwa kuendelea kutambua na kuunga mkono juhudi za maendeleo katika Jimbo la Kalambo, huku pia akiwashukuru wananchi wote walioshiriki katika kufanikisha ushindi wake.
Aeleza utekelezaji wa Ilani ndani ya miezi tisa
Mhe. Kanoni ameeleza mambo mbalimbali ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi yaliyofanyika katika kipindi cha miezi tisa tangu alipoingia madarakani, akieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kushughulikia changamoto na mahitaji ya wananchi wa Kalambo.
Ameomba Machifu pamoja na wananchi wote wa Kalambo kuendelea kushirikiana na kushikamana, akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni muhimu katika kuleta maendeleo ya Wilaya ya Kalambo.
Machifu wampongeza Mhe. Kanoni
Kwa upande wao, Machifu wa Wilaya ya Kalambo wamemshukuru Mhe. Kanoni kwa kutambua umuhimu wao na kuendelea kuthamini makundi mbalimbali ya kijamii katika utekelezaji wa majukumu yake.
Machifu hao wamempongeza kwa kazi wanazoeleza kuwa ni za kizalendo katika kuwatumikia wananchi na kushiriki katika juhudi za kuleta maendeleo Kalambo.
Aidha, wameahidi kuendelea kumpa ushirikiano katika kujenga Kalambo, huku wakimsihi aendelee kuwa kama alivyo sasa na asibadilike, pamoja na kuendelea kutatua changamoto za wananchi kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa kero.
Wasisitiza umuhimu wa Machifu katika jamii
Machifu wameeleza pia umuhimu wa viongozi wa kimila katika jamii, wakimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mfumo wa Machifu kama viongozi wa kimila.
Wamesema Machifu wana jukumu kubwa la kusaidia jamii kudumisha maadili mema yanayoendana na desturi na tamaduni za Kitanzania, pamoja na kushirikiana na Serikali katika kutatua migogoro mbalimbali, hususan migogoro ya ardhi ambayo wameeleza kuwa ni changamoto kubwa katika Wilaya ya Kalambo.
Wamueleza Mbunge changamoto ya usafiri
Pamoja na majukumu hayo, Machifu wameeleza kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu, hasa kutokana na changamoto ya usafiri inayowakabili katika kufika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kalambo.
Wameeleza kuwa Wilaya ya Kalambo ina kata 23 na vijiji 111, huku ikiwa na Machifu watatu pekee kwa wilaya nzima.
Kutokana na hali hiyo, wamemuomba Mhe. Kanoni kuwasilisha changamoto hiyo kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye wamemtaja kuwa Mkuu wa Machifu wote Tanzania, ili kusaidia kuweka mazingira bora ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mbunge kuendelea kukutana na makundi mbalimbali
Kikao hicho ni sehemu ya utaratibu unaoendelea wa Mhe. Kanoni wa kukutana na kusikiliza maoni na changamoto za makundi mbalimbali ya kijamii katika Jimbo la Kalambo.
Katika mwendelezo huo, tarehe 26 Septemba 2026, Mhe. Kanoni amepanga kukutana na vijana wa bodaboda wapatao 360, watakaowakilisha vijana kutoka kila kata ya Wilaya ya Kalambo.
Atoa wito wa kudumisha umoja na amani
Akihitimisha kikao hicho, Mhe. Kanoni amewaomba wananchi wa Kalambo kuendelea kudumisha upendo, mshikamano, umoja na amani, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kujenga Kalambo yenye maendeleo.
KAZI NA UTU TUNASONGA MBELE
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment