DODOMA: Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS), kwa niaba ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imetangaza nafasi 10 za ajira kwa Watanzania wenye sifa katika kada mbalimbali za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Tangazo hilo lenye kumbukumbu namba JA.9/16/01/54, limetolewa Septemba 1, 2026 na linawalenga wataalamu wenye uwezo, uadilifu, ari ya kufanya kazi na wanaozingatia matokeo.
Nafasi zilizotangazwa ni ICT Officer II (Software Development – Frontend) nafasi tatu, ICT Officer II (Software Development – Backend nafasi nne, ICT Officer II (Artificial Intelligence Applications) nafasi mbili, pamoja na ICT Officer II (Systems Analyst) nafasi moja.
NAFASI ZA SOFTWARE DEVELOPMENT – FRONTEND
PPRA imetangaza nafasi tatu za ICT Officer II – Software Development (Frontend).
Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Computer Science, Software Engineering, Information Technology, Information Systems, Computer Engineering au sifa inayolingana kutoka katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa.
Mwombaji anatakiwa kuwa na uzoefu wa vitendo katika miradi ya programu au kuwa na jalada linaloonyesha uwezo wake wa kutengeneza programu. Pia anapaswa kuwa na ujuzi katika teknolojia za kutengeneza mifumo ya wavuti kama Angular, TypeScript, HTML5, Tailwind CSS, Flexbox, CSS Grid na Angular Material.
Aidha, mwombaji anatakiwa kuwa na ujuzi wa kutengeneza programu zinazofanya kazi katika mifumo mbalimbali kwa kutumia Flutter na Dart, pamoja na uelewa wa REST APIs, GraphQL, Git, GitHub au GitLab. Ujuzi wa UI/UX na matumizi ya Figma au zana nyingine zinazofanana ni faida ya ziada.
NAFASI ZA SOFTWARE DEVELOPMENT – BACKEND
Nafasi nne za ICT Officer II – Software Development (Backend) zimetangazwa kwa wataalamu wenye Shahada ya Computer Science, Software Engineering, Information Technology, Information Systems au Computer Engineering kutoka taasisi inayotambuliwa.
Waombaji wanatakiwa kuwa na uwezo mkubwa katika Java 21 au zaidi, Spring Boot, Spring Data JPA na Hibernate, pamoja na uzoefu katika REST APIs, GraphQL, PostgreSQL, RabbitMQ na mifumo ya uchakataji wa taarifa kwa njia zisizofungamana moja kwa moja.
Ujuzi katika Kubernetes, Redis, Spring Security, OAuth2, JWT, JUnit 5, GraphQL na Postman utakuwa faida ya ziada.
NAFASI ZA ARTIFICIAL INTELLIGENCE
Kwa upande wa Artificial Intelligence Applications, PPRA imetangaza nafasi mbili.
Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Computer Science, Software Engineering, Artificial Intelligence, Data Science au taaluma nyingine inayohusiana na teknolojia.
Wanapaswa kuwa na ujuzi wa Python, TypeScript au JavaScript, pamoja na utengenezaji wa AI execution pipelines, RESTful APIs, JSON na mifumo ya uchakataji wa taarifa.
Pia wanatakiwa kuwa na uelewa au uzoefu wa kutumia mifumo ya Large Language Models (LLMs) inayoweza kuendeshwa kwenye kompyuta za ndani, ikiwemo Ollama, LM Studio, vLLM au LocalAI, au kutumia huduma za LLM zinazotolewa kupitia mifumo ya mtandaoni kama OpenAI, Gemini na Anthropic.
Waombaji pia wanatakiwa kuwa na uelewa wa prompt engineering, JSON schemas, function calling, tool use, agentic AI workflows, embeddings, vector databases na Retrieval-Augmented Generation (RAG).
NAFASI YA SYSTEMS ANALYST
Nafasi moja ya ICT Officer II – Systems Analyst imetangazwa.
Mwombaji anatakiwa kuwa na Shahada ya Computer Science, Information Systems, Information Technology, Software Engineering, Computer Engineering, Business Information Systems au taaluma inayolingana.
Mtaalamu huyo atahusika na uchambuzi wa mifumo na michakato ya biashara, ukusanyaji wa mahitaji ya watumiaji, uandaaji wa maelezo ya mifumo, nyaraka za kiufundi na miongozo ya watumiaji.
Pia atashiriki katika upimaji, utekelezaji, matengenezo na maboresho ya mifumo ya TEHAMA, kutoa msaada wa kiufundi kwa watumiaji, mafunzo, uchambuzi wa taarifa, uunganishaji wa mifumo na shughuli za uhakiki wa ubora.
Uelewa wa cyber security, enterprise applications na mifumo ya TEHAMA ya Serikali utakuwa faida ya ziada.
MSHAHARA
Nafasi zote 10 zilizotangazwa ziko katika daraja la mshahara PPRA 5.
MASHARTI YA JUMLA YA MAOMBI
Tangazo linaeleza kuwa waombaji wote lazima wawe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasizidi umri wa miaka 45.
Waombaji wanapaswa kuambatanisha nakala zilizothibitishwa za vyeti vyao vya elimu, ikiwa ni pamoja na shahada, diploma au vyeti vingine vinavyohitajika, pamoja na transcripts, vyeti vya usajili wa kitaaluma pale inapohitajika na cheti cha kuzaliwa.
Tangazo linasisitiza kuwa Form IV na Form VI results slips, testimonials pamoja na partial transcripts hazitakubaliwa.
Kila mwombaji anatakiwa pia kupakia picha ya hivi karibuni ya Passport Size katika mfumo wa maombi.
Watumishi walioajiriwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizo, na pia mtu aliyestaafu katika Utumishi wa Umma kwa sababu yoyote hatakiwi kuomba.
Mwombaji anatakiwa kutaja wadhamini watatu wanaotambulika pamoja na mawasiliano yao ya kuaminika.
Vyeti vya elimu vya nje ya nchi lazima vitambuliwe na mamlaka husika kama TCU, NECTA au NACTVET, kulingana na aina ya cheti.
NAMNA YA KUTUMA MAOMBI
Waombaji wanatakiwa kuandika barua ya maombi iliyosainiwa kwa Kiswahili au Kiingereza na kuiwasilisha kwa:
Secretary,
President's Office, Public Service Recruitment Secretariat,
P.O. Box 2320,
Mahakama Street, Tambukareli,
Dodoma.
Hata hivyo, maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia Recruitment Portal ya Sekretarieti ya Ajira.
Tovuti ya kutuma maombi: portal.ajira.go.tz
Mwombaji anaweza pia kuipata Recruitment Portal kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira kwa kuchagua sehemu iliyoandikwa “Recruitment Portal.”
MWISHO WA MAOMBI
Mwisho wa kutuma maombi ni Septemba 14, 2026.
Sekretarieti ya Ajira imesema ni waombaji watakaofaulu katika hatua ya usaili wa awali pekee ndio watakaojulishwa tarehe ya usaili.
Aidha, tangazo linaonya kuwa mtu atakayewasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo atachukuliwa hatua za kisheria.
Sekretarieti imesisitiza kuwa maombi yatakayowasilishwa kwa njia nyingine tofauti na Recruitment Portal hayatazingatiwa.
Imetolewa na:
Katibu, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment