Taarifa hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo imefuatia juhudi na maombi yaliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, kupitia Wizara pamoja na Bunge wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akiomba fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
Katika majibu yake, Serikali ilieleza kuwa fedha kwa ajili ya kukamilisha VETA Kalambo zingetolewa ifikapo Oktoba 2026. Hata hivyo, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imetekeleza ahadi hiyo kwa kutoa shilingi milioni 195, ambazo zimekwishawasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha mradi huo.
Ofisi ya Mbunge imetoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wote wa Serikali kwa kuendelea kuhakikisha fedha za miradi zinatolewa kwa wakati na kwa kuzingatia ahadi zinazotolewa kwa wananchi.
Ombi la kuongeza fedha ili VETA ianze kutoa mafunzo Januari 2027
Pamoja na fedha hizo kutolewa, Ofisi ya Mbunge imeiomba Serikali kuongeza fedha zaidi katika mradi huo ili kuwezesha kukamilika kwa VETA Kalambo kwa wakati na kutoa fursa kwa wanafunzi kuanza masomo ifikapo Januari 2027.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, changamoto iliyopo imetokana na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kupokea fedha kwa awamu sita, tofauti na mpango wa Serikali wa kutoa fedha kwa awamu saba, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya halmashauri nyingine.
Ofisi ya Mbunge imeeleza kuwa kukamilika kwa VETA Kalambo kutakuwa hatua muhimu katika kuwapatia vijana wa Wilaya ya Kalambo na maeneo jirani fursa ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi, hivyo kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Wito wa upendo, umoja na amani
Aidha, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalambo imeendelea kuwasihi wananchi wa Kalambo pamoja na Watanzania wote kudumisha upendo, mshikamano, umoja na amani kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Ofisi hiyo imesisitiza kuwa mshikamano na amani ni msingi muhimu wa kufikia malengo ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
“Tunawaomba Watanzania waendelee kuiamini Serikali ya Mama Samia kwa sababu inajibu kwa vitendo, si kwa maneno.”
Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.
Imetolewa na:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge, Jimbo la Kalambo


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment