KALAMBO, RUKWA — TAREHE 11 OKTOBA 2026
Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kalambo ameshiriki katika shughuli za kukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Kalambo tarehe 11 Oktoba 2026, ambapo Mwenge umetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi, kukabidhi vifaa kwa wananchi na vikundi, pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha huduma za jamii na kuinua uchumi wa wananchi.
1. KATA YA KANYEZI, KIJIJI CHA KANYEZI
Katika Kata ya Kanyezi, Kijiji cha Kanyezi, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule mpya ya sekondari. Hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za elimu na kuongeza fursa za wanafunzi kupata elimu katika mazingira bora.
Aidha, katika eneo hilo, Mwenge umekabidhi viti na meza za shule zilizotengenezwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB, Benki ya NMB na nguvu za wananchi. Vilevile, wananchi wamekabidhiwa majiko ya gesi na unga wa lishe kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuimarisha lishe katika jamii.
Katika ziara hiyo, Mwenge wa Uhuru pia umefungua ghala la mazao, hatua inayolenga kuimarisha uhifadhi wa mazao na kusaidia shughuli za kiuchumi za wananchi.
2. KATA YA ULUMI, KIJIJI CHA MNAZI
Katika Kata ya Ulumi, Kijiji cha Mnazi, Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi wa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000.
Taarifa iliyotolewa wakati wa ziara hiyo imeeleza kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 95. Kutokana na hali hiyo, maelekezo yametolewa kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa asilimia 100 ifikapo tarehe 30 Oktoba 2026 ili uweze kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Vilevile, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Zahanati ya Mnazi, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Katika kijiji hicho hicho, Mwenge wa Uhuru pia umeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Daraja la Mtula, ambalo linatarajiwa kurahisisha mawasiliano kati ya Kata ya Ulumi na Kata ya Mnamba. Kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kuongeza mwingiliano wa kijamii na kiuchumi, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi wa maeneo hayo.
3. KATA YA MAMBWEKENYA, KIJIJI CHA MADIBILA
Katika Kata ya Mambwekenya, Kijiji cha Madibila, Mwenge wa Uhuru umekabidhi trekta lenye thamani ya shilingi milioni 100, likiwa na tela pamoja na jembe, kwa kikundi cha vijana cha Tuinuane Group.
Trekta hilo limepatikana kupitia mkopo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Vijana, kwa lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali, hususan kilimo, na kuongeza fursa za kujikwamua kiuchumi.
Makabidhiano hayo yanaonesha umuhimu wa kuwawezesha vijana kupata zana za uzalishaji ili kuongeza tija katika kilimo na kukuza shughuli za kiuchumi katika jamii.
WITO WA OFISI YA MBUNGE KWA WANANCHI
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalambo inatoa shukrani za dhati kwa wananchi wote walioshiriki katika shughuli za Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Kalambo.
Ofisi inawapongeza wananchi kwa ushiriki wao na inaendelea kuwasihi kudumisha upendo, mshikamano, umoja na amani, ambazo ni nguzo muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kijamii na kuendeleza shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Kalambo.
Aidha, wananchi wanahimizwa kuendelea kushirikiana na viongozi katika kusimamia na kulinda miradi ya maendeleo ili iweze kutoa huduma zilizokusudiwa na kuwanufaisha wananchi wote.
IMETOLEWA NA:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kalambo
OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KALAMBO





💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment