KALAMBO, RUKWA.
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kalambo, Mhe. Edefonsi Joackim Kanoni, imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kujibu maombi ya Mbunge kwa vitendo kupitia utoaji wa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Matai–Tatanda–Kasesya.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mhe. Kanoni kuwasilisha maombi kupitia Bunge na Wizara husika akiomba Serikali itoe fedha kwa ajili ya kumlipa mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara hiyo, ambayo ni miongoni mwa miundombinu muhimu yenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Wilaya ya Kalambo na Taifa kwa ujumla.
Ofisi ya Mbunge imeeleza kuwa Serikali tayari imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara ya Tatanda–Kasesya, huku jitihada za kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kulipa deni lililobaki zikiendelea.
Aidha, Ofisi ya Mbunge imetoa shukrani za dhati kwa Serikali, Mawaziri na watendaji wote wa Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mhe. Kanoni katika juhudi zake za kuwasemea, kuwajali na kuwatetea wananchi wa Kalambo. Ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya Serikali na viongozi katika kuthamini mahitaji ya wananchi wa Kalambo na Watanzania kwa ujumla, pamoja na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ofisi ya Mbunge imewataka wananchi wa Kalambo kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kutambua dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Vilevile, wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Mbunge, Madiwani na watendaji wote wa Serikali katika ngazi mbalimbali ili kuimarisha ushirikiano na kuharakisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya Jimbo la Kalambo.
Ofisi ya Mbunge pia imewasihi wananchi kudumisha misingi ya upendo, umoja, mshikamano na amani, ikieleza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya jamii.
KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE.
IMETOLEWA NA:
Musa Frackison Mzopola
Katibu wa Mbunge
Jimbo la Kalambo.


💬 Toa Maoni Kuhusu Habari Hii
Umemaliza kusoma habari hii? Tupe maoni, mtazamo au swali lako hapa chini.
Comments
Post a Comment